BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange 'Kaburu'

UONGOZI wa klabu ya Simba umeingia anga za watani wao Yanga baada ya  kueleza hata wao wanajiandaa kukutana na Serikali kujadili na kutia saini makubaliano ya kutumia Uwanja wa Taifa pamoja na ule wa Uhuru baada ya ukarabati wa viti kukamilika.

Disemba 2 mwaka huu Yanga kupitia kwa Kaimu katibu mkuu wake Baraka Deusdedit alitia saini makubaliano na Katibu mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa na Utamaduni Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya Serikali kwa ajili ya kutumia Uwanja wa Taifa na Uhuru kwa ajili ya mechi za kitaifa na Kimataifa.

Mapema mwezi Oktoba Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye alizifungia timu za Yanga na Simba kutumia  Uwanja wa Taifa baada ya mashabiki wao kufanya vurugu kwenye mchezo baina yao ambapo viti 1,781 vilivunjwa pamoja na mageti manne ya kuingilia.

Makamu wa Rais wa klabu ya Simba Geofrey Nyange Kaburu amewaambia Waandishi wa Habari wakati akikagua ukarabati unaoendelea  wa viti hivyo ambavyo wanagharamia kila kitu unaotarajia kuchukua  wiki mbili kutoka sasa ili kukamilika kwakua mashabiki wao ndiyo walifanya tukio hilo lisilo la kiungwana licha ya kuchagizwa na maamuzi ya mwamuzi Martin Saanya kwenye mchezo wao wa Oktoba mosi dhidi ya Yanga.

"Kwa mujibu wa kanuni za ligi kila timu inatakiwa iwe na mkataba na Uwanja wanaoutumia, baada ya hatua hii ya ukarabati kukamilika tutakaa na Serikali kwa ajili ya makubaliano ya kutumia Uwanja huu na Uhuru kwa ajili ya mechi zetu za kitaifa na kimataifa," alisema Kaburu.

Tayari Saanya na msaidizi wake Samwel Mpenzu wameondolewa na Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF kuchezesha mechi za mzunguko wa pili kutokana na kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka kwenye mtanange huo ambao huvuta hisia za wapenzi wengi wa mpira ndani na nje ya Tanzania.

Post a Comment

 
Top