BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR
Rais wa Simba Evans Aveva akikabidhiana mkataba na Pastory Athanas

SIMBA imempa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji wa Stand United, Pastory Athanas huku Wekundu wakitakiwa kwenda kumalizana na 'Wapiga Debe' hao wa Shinyanga kwani bado ana mkataba na klabu hiyo.

Hata hivyo, Simba wamejipanga kwenda kumalizana na Stand muda wowote kwani tayari wameambiwa wawalipe Sh 10 milioni kwa ajili ya kuvunja mkataba wake ambao ulibaki wa mwaka mmoja.

BOIPLUS inafahamu kwamba hadi muda huu viongozi wa Stand wapo kwenye kikao wakijadili mambo mbalimbali ikiwemo usajili wao huku wakijadili suala la mchezaji huyo ambapo kocha wao Athman Bilali amekabidhi majina ya kikosi alichokipendekeza na jina la Pastory likiwa limekatwa.

Chanzo hicho kilisema kuwa Bilali amekuwa na msimamo kwamba mchezaji aliyeonyesha nia ya kuondoka kikosini mwake anamwachia ili aendelee na maisha nje ya timu yake kwa madai kuwa akimzuia anaweza kuharibu.

"Kikao kinaendelea cha viongozi, lakini jina la Pastory limekatwa kwenye majina tuliyoletewa na kocha Bilali nadhani ni kwa vile mchezaji mwenyewe alionyesha nia ya kutaka kuondoka. Kama amesajili Simba basi tutapaswa kulipwa kwani ana mkataba na sisi," kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho.

Ally Shomary

Mchana wa leo uongozi wa Simba ulipiga hodi kwa bosi wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser kwa ajili ya mazungumzo ya nyota wao wawili Ally Shomary pamoja na Rashid Mandawa mazungumzo ambayo yalianza tangu wiki iliyopita.

Chanzo cha ndani kutoka Simba kimeeleza kuwa tayari wamemalizana na Shomary baada ya Wekundu hao kushindwa kumnasa beki wa Prisons, Salum Kimenya aliyegoma kuachia ajira yake kwa usajili wa Sh 30 milioni walizotaka kumpa huku yeye akihitaji Sh 40 milioni.

Post a Comment

 
Top