BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu ya Azam Yahaya Mohammed  ameweka wazi kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kuisaidia timu hiyo kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Azam ndio wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano hiyo mwakani baada ya kuwa washindi wa pili katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) msimu uliopita ikifungwa na Yanga mabao 3-1 katika mchezo wa fainali.

Nyota huyo kwenye mechi yake ya kwanza kuichezea Azam alifanikiwa kufunga bao wakati Wana lambalamba hao   walipokuwa wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi iliyopita uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 bao jingine likiwekwa kimiani na winga Enock Atta Agyei.

Mohammed aliyesajiliwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo akitokea Aduana Stars ya Ghana alisema kuwa  atahakikisha anafunga mabao kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili kuweza kutimiza azma hiyo.

“Kombe la Shirikisho ni lengo langu kubwa, nataka kuisaidia Azam kuingia hatua ya makundi na mimi kuwemo kwenye kikosi kitakachoingia katika hatua hiyo malengo yangu makubwa yapo huko,” alisema Mohamed.

Azam imekuwa na kiu kubwa ya kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya miaka minne iliyoshiriki (mara moja Ligi ya Mabingwa na mara tatu Kombe la Shirikisho Afrika) kushindwa kufurukuta ambapo mwaka huu iliishia raundi ya pili baada ya kutolewa na vigogo wa Tunisia kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, ikishinda 2-1 nyumbani na kufungwa 3-0 ugenini.

Post a Comment

 
Top