BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
Hans Van der Pluijm

USIJICHORE mshua, nakushauri tena usijichore itakula kwako, nani alikudanganya bahati ya mtu hulaliwa mlango wazi?  Kila shetani na mbuyu wake 'braza' George. Kama huamini ngoja nikusimulie stori flani utanielewa.

Kuna mwanangu mmoja toka Tanga huko yalikozaliwa mapenzi, si unajua wale huwa hawajiulizi mara mbili linapokuja suala la kumdondokea mtu? Siku moja akaniibukia ''Ooh kaka, shemeji yako anataka nijichore tattoo yenye jina lake", nikamwambia kausha, biashara kichaa hiyo mwanangu.

Nikajiona nimemaliza kesi huku nikisahau kuwa wakiwa faragha siwi pamoja nao, mwanangu si akajichora bwana, tena ya kudumu, haikupita miezi miwili 'shemela' akampiga chini mwanetu na 'logo' yake kifuani.

Naamini alijifunza kuwa hizi tattoo bwana zinaweza kukupa mapenzi ya milele au zikafanya watu wakuchukulie poa kuwa huna ujanja tena, mwenzio Hans Pluijm tattoo yake imembeba vinginevyo alikuwa anaenda na maji, kapewa shavu la Ukurugenzi wa Ufundi, wazungu wenyewe wanafupisha kwa kuita TD.


Kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina

Ila kama wangeamua kumpotezea manake ingekuwa ngumu kupata 'ndoa' nyingine hapa Bongo, nani amuite wakati wanajua ana tattoo ya kijani na njano? Na si Bongo tu, timu nyingi za Afrika kwa ujumla sasa zinaogopa kuwapa kazi makocha walioonyesha mahaba ya wazi wazi kwa timu zao za zamani.

Nilishtuka sana niliposikia Babu kakubali kupewa kadi ya uanachama pale Jangwani (kajichora tattoo), ila baadae nikachukulia poa kuwa wamezidiana ujanja tu katika kutekana nyoyo, si unajua mjini mipango bwana. Ila uchovu ukanijia pale nilipokutana naye Diamond Jubilee siku ya uchaguzi mkuu wa Yanga.

Kabla sijajua kilichomleta mahali pale nikaona mshua anainuka kwenda kupanga foleni ya kupiga kura kama masihara vile, tena akitoka kwenye mazungumzo marefu na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti, Yusuf Manji.


Pluijm akiteta jambo na Yusuph Manji kabla hajaenda kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita wa Yanga

Nikajiuliza hivi uchaguzi ule ungekuwa na upinzani mkali kwenye nafasi ya Uenyekiti, tungetarajia Babu amchague mwingine tofauti na Bosi wake wa kipindi kile? Na kama ingetokea Manji akashindwa, bosi mpya angekubali kuendelea naye? Kwakweli hapa Babu alinitesa tu kwa maswali magumu wakati maisha yenyewe nayo magumu.

Lwandamina we usijichore tattoo bwana. Piga kazi uipe mafanikio Yanga utaheshimika na kukumbukwa milele, 'coaches are hired to be fired', hujui maisha baada ya Yanga yatakuwa wapi, na tottoo yako unadhani Azam watakufikiria? Utakatiza mitaa ya Msimbazi?, thubutu.

Kwanza usijisahau ukadhani kilichomuondoa Hans kwenye hicho kiti ulichokalia ni uwezo mdogo, la hasha. Huyo ni bonge la kocha, ndiye anashikilia tuzo ya kocha bora msimu wa 2015/16 na haikuwa kwa kubahatisha, kachukua 'ndoo' za Vodacom na FA, kafika raundi ya pili klabu bingwa Afrika lakini pia si unajua alitinga nane bora kombe la shirikisho Afrika?

Hayo ni mafanikio makubwa ambayo katika hali ya kawaida wengi tulidhani tajiri angempa fungu tu la kurekebisha kikosi chake, lakini kilichotokea ndo hiki. Labda walimchukulia poa, wamemzoea mwanafamilia mwenzao, ila ashukuru tattoo imempa nafasi ya kubaki katika nafasi nyingine, sijui ingekuaje laiti angepigwa chini kama mwanangu wa Tanga. Wewe usijichore mzee, mbuyu wa Pluijm si mbuyu wa Lwandamina.


E-mail; karim@boiplusmedia.com

Post a Comment

 
Top