BOIPLUS SPORTS BLOG


MANCHESTER UNITED KUNYAKUA WAWILI BENFICA

Klabu ya Man United ipo mbioni kuwanasa mabeki wa Benfica Victor Lindelof na Nelson Semedo katika dirisha dogo la usajiri la mwezi Januari.

Baada ya kufikia hatua nzuri ya makubaliano na beki  Lindelof  United wamehamishia nguvu za kumnasa  Semedo huku mazungumzo yakianza ya kumshawishi mchezaji huyo kujiunga na mashetani hao wa Old Trafford.

Semedo ataigharimu United paundi milioni 35 endapo Benfica watakuwa tayari kumuachia ingawa klabu hiyo  haijapanga kumuuza beki huyo mwezi Januari.


HART KUMRITHI COURTOIS CHELSEA

Kocha mkuu wa Chelsea Antonio Conte ameonesha nia ya kuwataka magolikipa kati ya Jan Oblak au Joe Hart  kuchukua mikoba ya Thibaut Courtois ambae anahusishwa na kujiunga na Real Madrid.

Kocha Conte yupo tayari kukubaliana na uhalisia wa kwamba golikipa wake Courtois anataka kutimka klabuni hapo na kujiunga na miamba hiyo ya soka ya Hispania katika majira ya joto ya mwaka 2017.

Oblak amepata majeraha yatakayo mfanya akae nje ya uwanja miezi mitatu huku Hart akimalizia muda wake wa mkopo katika timu ya Torino inayoshiriki ligi kuu nchini Italia.


BEIJING GUOAN YAMTENGEA OFA PODOLSKI

Klabu ya Galatasaray ya Uturuki imeweka wazi kuwa mshambuliaji wao Lucas Podolski huenda akatimkia katika klabu ya Beijing Guoan ya China.

Podolski ambaye amebakisha mkataba wa miaka mitatu na miamba hiyo tangu ajiunge nao mwaka 2015 huenda akafikiria ofa hiyo kama ikiwasilishwa  baada ya klabu za China kuanza kuvutia wachezaji wenye majina makubwa.

Tayari wachezaji kama Oscar na CarlosTevez wamesaini na klabu za China mapema mwezi huu huenda wakajiunga na wachezaji kama Pepe, Podolski, Cesc Fabregas ambao wanahusishwa na uhamisho kuelekea huko.


MAN UTD,LIVERPOOL NA ARSENAL WAPIGANA VIKUMBO KWA BRANDT

Baada ya winga wa Bayern Leverkusen Julian Brandt kuwa na msimu mzuri amezifanya klabu za ligi kuu nchini Uingereza kuhitaji huduma yake katika dirisha la usajili la mwezi Januari.

Winga huyo ambae alikua akihusishwa na Arsenal na Liverpool hatimaye United wamejiunga katika kinyang'anyiro hicho cha kupata saini ya kinda huyo.

United inategemea kuongeza kasi katika mchakato huo ili kuwapiku Arsenal na Liverpool ambao walianza mchakato huo  mapema.

Brandt  amechezea mechi 80 na kufunga mabao 17 akiwa na rekodi bora  akizidiwa idadi ya pasi za mwisho na Ousmane Dembele na Emil Forsberg wa RB Leipzig. 


KINDA WA MADRID KUTUA AJAX

Baada ya kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha Real Madrid kinda Martin Odegaard huenda akatimkia Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

Wawakilishi wa Odegaard wameonekana katika jiji la Amsterdam huku ikiaminika kuwa wameenda kufanya mazungumzo na klabu ya hiyo ili wamchukue kwa mkopo.

Odegaard ambaye alijiunga na  Madrid mwaka 2015 amecheza mechi mbili pekee akiwa na kikosi cha kwanza huku  akilipwa paundi 80,000 kwa wiki na huenda akapata nafasi zaidi katika klabu hiyo kama uhamisho wake ukifanikiwa.


BAKAYOKO AKANUSHA KUTIMKA MONACO

Kiungo wa AS Monaco Tiemoue Bakayoko ambaye anahusishwa na kujiunga na klabu za Chelsea na Manchester United amekanusha taarifa za kuondoka kwa miamba hiyo ya Ufaransa.

"Mwanzoni mwa msimu wazo la kuondoka lilikuja ila sikujua klabu ipi ingenifaa mpaka pale kocha aliponifanya kuwa mchezaji muhimu nikabadili mawazo marafiki waliniambia kuhusu habari za kuhusishwa na klabu nyingine ila sizifatilii maana sitaondoka Monaco Januari" alisema Bakayoko.

Bakayoko  ameisaidia Monaco kukwea hadi nafasi ya pili katika msimamo  wa ligi kuu Ufaransa na  kufunga magoli mawili katika mechi 16 za ligi huku akitabiriwa kuwa  mbadala wa Michael Carrick atakapotimka United.

Imeandaliwa na Abra David Jr kwa msaada wa mitandao

Post a Comment

 
Top