BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
AZAM FC wana mpango wa kumsainisha winga Hassan Kabunda wa Mwadui FC lakini uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake mjini Shinyanga umesema kwamba acha aondoke kwani tayari wamempata Awadh Juma wa Simba ambaye anaweza kucheza nafasi yake.

Awadh hajacheza mechi hata moja kwenye kikosi cha kocha Joseph Omog tayari yupo mjini Shinyanga na ameanza mazoezi na kikosi hicho kilicho chini ya kocha mpya, Ally Bushiri. Awadh ametua Mwadui kwa mkopo wa miezi sita.

Mbali na Awadh pia mchezaji wa Simba, Malika Ndeule amerudi kwenye kikosi chake hicho baada ya kusoma alama za nyakati kuwa ndani ya Simba kuna ushindani mkubwa wa namba na hivyo alikuwa akiishia benchi ama jukwaani kama ilivyokuwa kwa Awadh.

Katibu Mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao ameiambia BOIPLUS kuwa wamemrudisha nyota wao Razak Khalfan aliyekwenda Singida United huku wakiwa katika hatua za mwisho za kumpa mkataba straika wa Yanga, Matheo Anthony aliyemaliza mkataba na Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom.


"Tukimpata Matheo tutakuwa tumefunga usajili maana tumezungumza naye tayari na kesho Ijumaa ndiyo tutafikia makubaliano ya mwisho. Azam walizungumza na sisi kuhusu Kabunda ila hawakuja rasmi hivyo kama wanataka kumsainisha waje tumalizane sisi hatuna tatizo kwani tayari yupo Awadh anayeweza kucheza nafasi yake.

"Mfumo wa kocha wetu hauwezi kusumbua kutokuwepo kwa Kabunda ndiyo maana nasema hata akiondoka hakuna shida kikosi chetu tumekiimarisha kila idara kwa sasa," alisema Kilao.

Habari za chini ya kapeti zinasema kwamba tayari Azam wamempa mkataba Kabunda huku Joseph Mahundi akisubiri kocha wa matajiri hao, Zeben Hernandez arejee kutoka kwenye mapumziko.

Mahundi kwasasa imeelezwa yupo jijini Mbeya na uongozi wa klabu ya Mbeya City umemtaka ajiunge na wenzake mazoezini ili wazungumze juu ya mkataba mpya hata kama Azam watamfata hapo baadaye hawatakuwa na tatizo.

Post a Comment

 
Top