BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
SIMBA bado haijaweka wazi wachezaji gani wanaweza kuachwa kwenye usajili wa dirisha dogo unaoendelea lakini ujio wa kipa kutoka Ghana, Daniel Agyei ambaye leo Alhamisi alitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba umebadili kila kitu na kuna uwezekano Vincent Angban akapigwa chini huku Manyika Peter Jr akishauriwa pia kuondoka.

Angban amebakiza mkataba wa miezi sita, Musa Ndusha bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu sasa kwani alisaini mkataba wa miaka miwili na inasemeka anaweza kupelekwa kwa mkopo pamoja huku pia kukiwa na uwezekano mkubwa wa Janvier Bokungu ambaye mkataba wake unamalizika mwezi huu kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Wakati Agyei aliyetokea timu ya Medeama akiandaliwa kwa ajili ya vipimo, kocha wa zamani wa makipa, Idd Pazi amemtaka kipa Manyika Jr kuachana na Simba na kwenda kutafuta maisha ya soka sehemu nyingine ambako atakapata nafasi ya kucheza ili kulinda kipaji chake.

Pazi aliiambia BOIPLUS kuwa taratibu za usajili wa wachezaji zinaruhusu mchezaji ambaye hajacheza mechi za mzunguko wote wa kwanza kuomba kwenda kwa mkopo ama kuvunja mkataba ili kulinda kiwango chake hivyo Manyika ambaye anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Angban ambaye pia ameletewa mpinzani wake anaweza kufanya maamuzi hayo.


"Nitapiga kelele siku zote kuhusu kipaji cha Manyika Jr, ni kijana mwenye kipaji ila alikosa mwongozo hapo awali. Ninachotaka kumwambia Manyika ni kwamba aachane na Simba atafute timu nyingine ili acheze kwani kiwango kinashuka kwa kukang'ang'ania kukaa sehemu ambayo hupati nafasi. Manyika asome alama za nyakati, dalili zilijionyesha muda mrefu kuwa nafasi kwake ni finyu.

"Najuwa wachezaji wengi wakitoka Simba na Yanga wanajiona wanyonge kucheza timu hizi za kawaida lakini waangalie mwenzao Juma Kaseja amecheza Simba miaka mingi lakini alijikubali kutoka Dar es Salaam kwenda kupambana mikoani na anaonekana, Manyika afanye hivyo maisha sio Simba pekee," alisema na kuongeza.

"Hata Ivo Mapunda alitoka Yanga alienda nje baada ya kuona kiwango chake kimeshuka, alifanya vizuri na akarudi kwenye kiwango bora Simba wakamfuata lakini cha kusikitisha sasa hivi sijui hata alipo ingawa bado naamini uwezo wake ni mkubwa. Tatizo la viongozi wa klabu ni kushindwa kuwa na watu wanaowafuatilia wachezaji huku kila mmoja akitaka kumsajili mchezaji aliyempenda na ndiye atapata nafasi ya kucheza," alisema Pazi.

Rais wa Simba, Evans Aveva alisema kuwa, "Atafanyiwa vipimo vya afya halafu tutamsubiri koha Joseph Omog ambaye atawasili kesho Ijumaa ili awepo ndipo tumpe mkataba,".

Hadi sasa Simba ina wachezaji saba wa kigeni ambao ni Angban, Juuko Murshid, Bokungu, Mwanjali, Ndusha, Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon ambayo ni idadi iliyopitishwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Post a Comment

 
Top