BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
UONGOZI wa Klabu ya Simba leo Jumamosi ni kama umewashitaki wachezaji wao Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu kwa wanachama baada ya kudaiwa kuwa wanagoma kusaini mikataba mipya.

Mkude na Ajibu mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu lakini tangu viongozi wa Simba waanze kuzungumza nao kwa ajili ya mikataba mipya hakuna hata mmoja aliyekubali kusaini huku wakitajwa kujiunga na timu nyingine hususani Yanga.

Katika kikao cha siri kilichofanyika kwenye ukumbi wa klabu hiyo uliopo Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam viongozi wa Simba na viongozi wa matawi walielezea juu ya mchakato mzima wa usajili huku wakisema straika mmoja atawasili pamoja na kocha Joseph Omog kati ya leo usiku ama kesho.

Mpaka sasa Simba imemleta kipa kutoka Ghana, Daniel Agyei  aliyekuwa akiichezea Medeama ambaye jana Alhamisi alitarajiwa kufanyiwa vipimo ndipo asaini mkataba.


  • Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa viongozi hao hawakutaka  kuzungumzia zaidi juu ya tamko la Mwenyekiti wa Baraza la Udhamini, Hamis Kilomoni ingawa walielezea ajenda zao tu ambazo zitajadiliwa siku ya mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Desemba 11 kwenye Ukumbi wa Bwalo la maafisa wa Polisi, Oysterbay.


"Kikao hakikuwa na kitu cha ziada ila tumeleezwa mchakato wa usajili ulivyo na jinsi Mkude na Ajibu wanavyosumbua kwenda kuongeza mikataba. Wametueleza wanachama na kwamba wanaendelea kuzungumza nao.

"Sisi tumewaambia kama hawataki waachane nao ili wamalize mikataba yao mwishoni mwa msimu huenda wana malengo mengine na kuendelea kumlazimisha mtu ambaye hataki ni sawa na kutwanga maji kwenye kitu, viongozi wakiona imeshindikana waachane nao," kilisema chanzo hicho.

Akizungumza wakati wa kikao hicho na viongozi wa matawi ya Simba, Rais Evans Aveva aliwasomea ajenda za mkutano huo pamoja na maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi huku akiwapa nyaraka za mkutano huo ili wazipitie.

Post a Comment

 
Top