BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR
 Video ikionyesha uwezo wa James Kotei uwanjani

KLABU ya Simba inatarajia kushusha kiungo mkabaji kutoka Ghana, James Agyekhum Kotei ambaye atataua nchini muda wowote kuanzia sasa.

Kwa mara ya mwisho Kotei aliichezea timu ya Al Oruba ya Oman ambayo ilishindwa kumlipa pesa ya usajili na kuamua kuachana nayo.

Kotei mwenye umri wa miaka 23 anatua Simba kumpa changamoto Jonas Mkude ambaye hajasaini hadi sasa kukiwa na habari ya kuwa anataka kwenda kuitumikia Yanga ama kwenda nje ya nchi mara mkataba wake utakapomalizika.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kilisema kuwa kiungo huyo amefanya mazungumzo ya awali na Simba ambao wamechunguza na kuona ana kila sifa itakayomuweka benchi Mkude aliyegoma kusaini mkataba mpya. Kotei akitua atafanyiwa vipimo ndipo asaini mkataba kama watafikia makubaliano ya mwisho.


"Mkude anaringa kwa vile ameona hana mpinzani wa kumuweka benchi ndiyo maana wameona walete mchezaji wa kigeni atakayempa changamoto ili hata akiondoka tusiwe na pengo. Maana kinachoendelea kwa sasa hatabembelezwa tena hadi atakapoamua mwenyewe," kilisema chanzo hicho.

Kotei atakuwa ni mchezaji wa pili kutoka Ghana baada ya uwepo wa kipa Daniel Agyei aliyetokea timu ya Medeama. Kipa huyo anatajwa kuchukuwa nafasi ya Vincent Angban kama watafikia maamuzi ya kumvunjia mkataba wake uliobaki miezi sita.

Hadi sasa Simba ina wachezaji saba wa kigeni ukiachana na Angban wengine ni Juuko Murshid, Method Mwanjali, Musa Ndusha, Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon na Janvier Bokungu.

Habari za ndani zinasema kuwa Bokungu, Musa na Angban ndio waliokalia kuti kavu wakati Juuko anaweza kuuzwa nje ya nchi na kwamba huenda beki huyo kutoka Uganda asiwe na kikosi cha Simba kwa miezi miwili.

Post a Comment

 
Top