BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
UMOJA wa vijana wa klabu ya Simba kesho Jumapili utafanya bonanza maalum lililopewa jina la 'Nyekundu na Nyeupe' litakalohusisha vijana wa timu hiyo kutoka sehemu mbali mbali za jiji la Dar es Salaam litakalofanyika CDS Park Chang'ombe (TTC CLUB) kuanzia saa nne asubuhi.

Lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha vijana kutambuana na kujadili masuala mbali mbali ya kimaendeleo ya klabu yao pamoja na kuhamasisha umoja imara ambao utaongeza mshikamano ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Bonanza hilo litapambwa na mechi kali kati ya kundi mama la vijana wa Simba (UVSSC) dhidi ya 'Simba Sporaa' mchezo ambao unatarajiwa kuwa mkali kutokana na timu zote mbili kufanya maandalizi ya kutosha huku zikijinasibu kutoka na ushindi katika mtanange huo.


Wachezaji wa timu ya Simba Sporaa wakijiandaa kuanza mazoezi

Makamu Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa timu hiyo Abeid King Mswati ameiambia BOIPLUS kuwa katika bonanza hilo hakutakuwa na kiongozi yoyote kutoka kwenye uongozi wa juu kutokana na makundi yaliyopo ndani ya klabu hiyo na wao wasingependa kuwa upande wowote.

"Hakutakuwa na kiongozi yoyote kutoka kwenye uongozi kutokana na makundi yaliyopo sisi hatutaki kuwa upande wowote," alisema Mswati.

Mswati alienda mbali zaidi kwa kusema wanataka umoja huo utambulike kwenye katiba ya klabu hiyo ili wawe na maamuzi katika masuala mbali mbali kwakua wao ni kundi kubwa na ndiyo nguvu kazi.

Post a Comment

 
Top