BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR

WACHEZAJI wa Yanga leo wameendeleza mgomo wao kwa kutofanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ijayo dhidi ya African Lyon, mechi hiyo itachezwa Ijumaa, Uwanja wa Uhuru.

Mgomo huo ambao ulianza jana Jumatatu katika mazoezi yaliyopaswa kufanyika Uwanja wa Uhuru ni kwa lengo la kushinikiza uongozi uwalipe mshahara wao wa mwezi Novemba.

Leo Jumanne asubuhi kocha mkuu, George Lwandamina alikiamsha kikosi chake kama kawaida ili kuwapa mbinu mpya kuelekea mechi hiyo lakini wachezaji wake wachache waliofika uwanjani hawakuonyesha kujali wala kuwa na hofu kwa kugomea mazoezi hayo.

Lwandamina alilazimika kukiondoa kikosi hicho uwanjani bila kufanya mazoezi ikiwa ni siku ya pili sasa ambapo kilionekana kuwa na wachezaji  wachache ambao hawakushuka hata kwenye Basi lao.

Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Deusdetit Baraka amekiri kuwepo na tatizo hilo la kutolipa mshahara wa Novemba na kuelezea kuwa suala hilo linashughulikiwa ambapo watalipa muda wowote kuanzia sasa kabla ya mechi hiyo.

"Hili suala tutalitatua muda wowote kuanzia sasa, hivyo kila kitu kitakuwa sawa kuelekea mechi ijayo," alisema Baraka.

Post a Comment

 
Top