BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
NYOTA wa tano wapya waliosajiliwa dirisha dogo la usajili lililopita wameshindwa kuisaidia Azam FC kuibuka na pointi tatu baada ya kulazimishwa sare tasa na African Lyon, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Uhuru.

Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez alishuhudia vijana wake wakipambana yeye akiwa jukwaani kwani anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu.

Nyota wapya walioanza mchezo huo ni Yakubu Mohamed, Yahaya Mohamed, Joseph Mahundi, Samwel Affoul pamoja na Stevin Kingue bado wana kazi kubwa kuhakikisha wanaisaidia Azam kufanya vizuri mzunguko huu wa pili wa ligi.

Mchezo huo haukuwa na kasi kubwa kama matarajio ya wengi huku Azam wakicheza vizuri kuanzia nyuma lakini kutokuwa makini kwa upande wa safu ya ushambuliaji kuliwakosesha mabao kipindi cha kwanza.

Azam walifanya shambulio kali langoni mwa Lyon ambapo nahodha John Bocco alipiga shuti lililopanguliwa na mlinda mlango Youth Rostand baada ya kupokea krosi ya Shomari Kapombe.


Mshambuliaji Yahaya alifunga bao kwa Azam dakika ya 72 lakini mwamuzi Hans Mabema kutoka Tanga alilikataa baada ya kuumizwa kwa mlinda mlango Rostand.

Mwamuzi aliwaonya kwa kadi ya njano Omary Salum kwa upande wa Lyon huku Agrey Moris na Yakubu nao wakipewa kwa Azam.

Lyon iliwatoa Fredy Cosmas, Abdallah Mguhi na Rostand nafasi zao zikachukuliwa na Omary Abdallah, Raizani Hafidh pamoja na Salehe Malande. Azam iliwapumzisha Samwel Affoul, Bruce Kangwa na Joseph Mahundi ambapo Frank Domayo, Aboubakari Salum pamoja na Ramadhani Singano walichukuwa nafasi hizo.

Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Prisons walioikaribisha Majimaji waliibuka na ushindi wa bao 1-0, bao la Prisons lilifungwa na Victor Hangaya dakika ya 68.

Hangaya alifunga bao hilo kwa shuti kali ambalo lilisababishwa na krosi iliyopigwa na Benjamin Asukile.

Post a Comment

 
Top