BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, MTWARA
WAMEREJEA!, wekundu wa Msimbazi Simba wameonyesha kuwa wao si watu wa 'mchezo mchezo' baada ya leo kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu kwa kuikandamiza Ndanda mabao 2-0 kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Simba ambao jana walishushwa na mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 36  walipata mabao yao kupitia kwa Mzamiru Yassin dakika ya 63 na Mohamed Ibrahim dakika ya 81 hivyo kujihakikishia ushindi uliowarejesha kileleni kwa kufikisha pointi 38.

Simba walionyesha uwezo mkubwa hasa katika eneo la kiungo ambapo Mzamiru aliyeingia badala ya James Kotei aliyeumia alishirikiana vema na Jonas Mkude katika eneo la kati huku kuingia kwa Said Ndemla kukiwavuruga zaidi 'Wanakuchele' hao ambao hawakuwa na cha kufanya ili kuwazuia Simba wasipate mabao.

Kipa mpya Daniel Agyei alionyesha umahiri kwa kuokoa hatari kadhaa na kufanikiwa kuwaondoa patupu washambuliaji wa Ndanda walioongozwa na Omari Mponda.


Post a Comment

 
Top