BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, MBEYA

MBEYA City leo imepata ushindi wa kwanza katika mzunguko wa pili wa ligi kuu huku mshambuliaji mpya Zahoro Pazi akitokea benchi na kuwaonyesha mashabiki alivyou'miss mpira kwa kutupia bao la tatu na la kwanza tangu apate ITC yake katika mechi ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbao FC mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine.

Zahoro alifunga bao hilo baada ya kuwachambua mabeki wanne wa Mbao FC kisha kupiga shuti kali ambalo lilitinga wavuni huku akipewa kadi ya njano kwa kuvua jezi alipokuwa akishangilia bao lake hilo alilofunga dakika 80.

Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri alimuingiza Zahoro kuchukuwa nafasi ya Ayoub Sentawa pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyechukuwa nafasi ya Raphael Bryson.Mabao mengine ya Mbeya City yalifungwa na Rafael Daud dakika ya 23 aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Rafael Bryson huku bao la pili likifungwa kwa penalti na Mganda, Tito Okello aliyechezewa rafu na kipa wa Mbao, Emmanuel Mseja, bao hilo lilifungwa dakika ya 33 huku kipa huyo akipewa kadi ya njano.

Mbao ndio walikuwa wa kwanza kuliona lango la wenyeji wao dakika ya 19 kupitia kwa mchezaji wao Rajeshi Kotecha ukiwa ni mpira wa kurusha na kumkuta mchezaji huyo aliyewachambua mabeki wa City na kutikisa nyavu.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo Zahoro alisema kuwa; "Namshukuru Mungu na kocha kwa kuniamini na kunipa nafasi naamini nitafanya vizuri zaidi siku zijazo na nitakuwa nimezoea mfumo,".

Post a Comment

 
Top