BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya Simba Zahoro Pazi ameliomba Shirikisho la mpira wa miguu TFF kumsaidia kuipata hati yake ya uhamisho ya Kimataifa (ITC)
iliyozuiwa na timu ya FC Lupopo ya Congo kwa madai ya kuwa wana mkataba wa miaka mitatu na mchezaji huyo.

Zahoro anatakiwa na timu ya Mbeya City kwenye dirisha hili dogo la usajili lakini kama hati hiyo haitapatikana ina maana atashindwa kujiunga na 'Wagonga Nyundo' hao wa jiji la Mbeya.

Tayari mshambuliaji huyo amekaa miaka miwili bila kucheza mpira huku akikiri kuwa soka ndiyo ajira yake anayoitegemea na kuendelea kukaa bila kucheza kunazidi kumpotezea malengo aliyojiwekea.

Zahoro ameiambia BOIPLUS kuwa mara kadhaa ameenda katika ofisi za TFF kuomba msaada wa kuipata ITC yake kutoka Lupopo lakini amekuwa akizungushwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.


"Mi nawaomba TFF wanisaidie kuipata ITC yangu iliyozuiwa Lupopo kwakua naendelea kukaa bila kucheza mpira wakati ndiyo ajira yangu inayoniweka mjini lakini msaada wao kwangu ni mdogo au hamna kabisa," alisema mtoto huyo wa kipa wa zamani Idd Pazi.

Zahoro amepinga vikali kusaini mkataba na Wakongomani hao kwa maelezo kuwa alitakiwa kwenda kufanya majaribio tu lakini cha kushangaza aliambiwa amesaini huku akioneshwa mkataba feki ambao yeye mwenyewe hautambui.

"Mimi sijawahi kusaini mkataba na Lupopo walinitaka nikafanye majaribio na nilienda mazoezini siku moja tu tukashindwana nikarudi nyumbani nashangaa kusikia ITC yangu imetumwa huu ni mchezo mchafu nimechezewa," alisema mshambuliaji huyo.

Msimu uliopita timu ya Polisi Morogoro inayoshiriki ligi daraja la kwanza ilikuwa ikihitaji huduma yake lakini kutokana na kukosekana na ITC yake alishindwa kusajiliwa hali ambayo inaweza ikajitokeza kwenye usajili wake wa kwenda Mbeya City.

Post a Comment

 
Top