BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu, Zanzibar
TIMU ya Azam imeonyesha bado haiko sawa baada ya leo kubanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Jamhuri kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar mtanange uliofanyika kwenye uwanja wa Amani.

Kipa wa timu ya Jamhuri Ally Suleiman Mrisho amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi baada ya kuokoa michomo kadhaa ya wachezaji wa Azam.

Jamhuri walicheza kwa utulivu na kujiamini ili kuhakikisha ile dhahama ya mabao 6-0 waliyofungwa na Yanga kwenye mchezo wao wa ufunguzi haijirudii tena.

Mshambuliaji Yahaya Mohammed alikosa bao la wazi dakika tatu kabla ya timu hizo kwenda mapumziko huku Azam wakifika zaidi langoni mwa Jamhuri lakini suala la umakini lilikuwa changamoto kubwa kwao.

Winga mpya wa klabu hiyo Enock Agyei aliyesajiliwa kutoka timu ya Medeama ya Ghana alitolewa dakika ya 44 kumpisha Ramadhan Singano baada ya kuonekana kushindwa kufurukuta mbele ya Wanzibar hao.

Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu ila tatizo la umaliziaji liliendelea kuwa changamoto ambapo Jamhuri walijitahidi kuwadhibiti wachezaji wa Azam waliokuwa wakitafuta bao kwa kila hali.

Post a Comment

 
Top