BOIPLUS SPORTS BLOG


Mwandishi wetu, Zanzibar
YANGA walikuwa wanaichukulia poa Azam FC hasa kutokana na kusuasua katika michezo yao ya hivi karibu huku wao wakitisha visiwani kwa kugawa dozi hapa, lakini usiku huu Wanalambalamba hao wameonyesha kasi yao ni 4G baada ya kuibamiza Yanga mabao 4-0 kwenye mchezo wa mwisho kundi B wa kombe la Mapinduzi uliofanyika Uwanja wa Amani.

Nahodha John Bocco 'Adebayor' aliipatia Azam bao la mapema dakika ya pili ya mchezo baada ya shuti la mguu wa kushoto lililopigwa na winga Joseph Mahundi kupanguliwa na mlinda mlango Deogratius Munishi 'Dida' kabla ya kumkuta mshambuliaji huyo.

Katika kipindi cha kwa kwanza cha mchezo huo uliokuwa wa kasi, Azam walifanya mashambulizi ya hatari langoni mwa Yanga mara tatu huku mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Vodacom wakifanya hivyo mara moja pekee.

Yahaya Mohammed aliipatia Azam bao la pili kwa kichwa dakika ya 54 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Abubakar Salum 'Sure Boy' ambaye alionyesha kiwango cha juu leo.

Mahundi alifunga bao la tatu dakika ya 80 kwa shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la 18 baada ya kupokea pasi nzuri toka kwa Gadiel Michael. Shuti lilimuacha Dida akichupa bila mafanikio.

Enock Atta Agyei aliyetokea benchi alihitimisha karamu ya mabao baada ya kufunga bao nne dakika ya 84 akitumia vyema makosa ya Geofrey Mwashiuya aliyeshindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Mahundi.

Kwa matokeo hayo Azam imeongoza kundi B ikiwa na pointi saba huku Yanga wakishika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi sita. Timu hizo zinasubiri mechi za mwisho za kundi A hapo kesho  ili kujua watapambana na nani kwenye hatua ya Nusu fainali.

Post a Comment

 
Top