BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar

BEKI wa zamani wa Simba na Mbeya City, Juma Nyosso jana Jumatano aliwasilisha barua nyingine katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuomba apunguziwe adhabu yake aliyofungiwa kucheza soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili.

Wakati Nyosso akipeleka barua hiyo ambayo ni ya tatu bila kusikilizwa kilio chake aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro naye amewasilisha maombi ya kupunguziwa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja kutojihusisha na soka.

Nyosso alifungiwa baada ya kumfanyia kitendo cha utovu wa nidhamu mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco ambapo sasa adhabu yake inatarajiwa kumalizika Oktoba wakati Muro alipewa adhabu hiyo mwaka jana baada ya kutoa lugha chafu kwa vigogo wa TFF.

Habari kutoka ndani ya TFF zinasema kuwa kesho Ijumaa, Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi za wachezaji huenda ikakutana na kuelezwa kuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni kuhusiana na barua hizo na kuzitolea maamuzi kama watapunguziwa adhabu ama kuondolewa kifungoni.

Mwaka jana Nyosso aliwasilisha barua mbili za kujutia kitendo chake hicho ambapo TFF haikujadili barua hata moja na kwamba beki huyo hakukata tamaa hadi jana alipowasilisha barua nyingine.

"Hii ni barua ya tatu kuwasilisha naamini ipo siku watanielewa na kunisamehe ili nitoke kifungoni, kazi yangu ni mpira na ndiyo ilikuwa inaendesha maisha yangu pamoja na familia inayonitegemea lakini kwasasa maisha kwangu yamekuwa tofauti," alisema Nyosso.


Kwa upande wa Muro yeye aliandika barua yake Januari 2, ambapo kifungo chake kilianza Julai mwaka jana na hivyo amebakiza miezi saba kwenye kifungo chake tofauti na Nyosso ambaye amebakiza miezi 10 kwani alifungiwa Oktoba mwaka juzi.

Post a Comment

 
Top