BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi,Dar

KOCHA wa timu ya JKT Ruvu, Bakari Shime ameiongoza timu hiyo mechi tatu sasa lakini bado hajapata ushindi wowote katika mechi hizo tangu achukue mikoba iliyoachwa na Malale Hamsini kwani leo Jumapili ameambulia sare tasa dhidi ya African Lyon.

Mechi hiyo ambayo ni mwendelezo wa mechi za ligi kuu ya Vodacom imechezwa Uwanja wa Uhuru na kuifanya Lyon ifikishe pointi 20 wakati Maafande hao wakikusanya pointi 14 huku wakishika mkia.

Lyon imekuwa na muendelezo mzuri katika uwanja wa Uhuru baada ya kuwabana Azam FC wiki mbili zilizopita huku wakionekana kucheza mpira wa kujilinda zaidi na kushambulia mara chache lakini kwa mipango.

Dakika ya 26 mshambuliaji Saady Kipanga alikosa goli la wazi baada ya kucheza kwa maelewano mazuri na Hassan Matelema lakini shuti lake alilopiga ndani ya eneo la hatari lilipaa juu ya lango la Lyon.

Ruvu walishambulia zaidi ya Lyon lakini umakini wa safu ya ulinzi ya vijana hao wa Temeke ambayo huzisumbua timu mbalimbali uliwanyima nafasi Maafande hao ya kupenya ngome hiyo hivyo kuambulia pointi moja.


Akizungumza mara baada ya mechi hiyo Shime alisema kuwa, "Kupata pointi moja kwetu kuna maana kubwa sana, niliikuta timu ipo chini sana na hata sasa ipo chini ila kuna mabadiliko makubwa, leo tumeshambulia sana lakini hatukuweza kufunga.

"Sisi hatuendi mapumziko na hatuna muda wa kupumzika kwani tupo chini hivyo tunaendelea na maandalizi yetu kama kawaida, tunafahamu hata tutakaocheza nao siku zijazo nao wanajiandaa hivyo lazima tuendelee na maandalizi yetu," alisema Shime.

Shime alisema anapambana kuhakikisha anaitoa timu kwenye nafasi iliyopo hivyo bado anaona kama yupo vitani kwenye ligi kuhakikisha lengo lake linatimia.

Stand United yenyewe imeendelea kupoteza mechi zake baada ya leo kuambulia kipigo cha bao 2-1 mechi iliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Post a Comment

 
Top