BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu,Zanzibar

JANVIER Bokungu ameingia rasmi kwenye orodha ya mashujaa wa timu ya Simba baada ya kuisaidia kutinga fainali ya kombe la Mapinduzi kwa kuwafunga watani wao wajadi Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2 kutokana na sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili iliyopigwa uwanja wa Amani.

Licha ya kufunga penati ya ushindi, beki huyo mtulivu aliokoa mipira miwili iliyokuwa ikielekea nyavuni huku pia akizuia krosi kadhaa ambazo zingeweza kuwa na madhara langoni mwao.

Mlinda mlango Daniel Agyei aliokoa penati mbili zilizopigwa na Deogratius Munishi na Mwinyi Haji huku mwenyewe akifunga mkwaju wa pili. Beki Method Mwanjale alikosa mkwaju wake kwa upande wa Simba.

Nahodha Jonas Mkude na Mzamiru Yassin wao walifunga penati zao huku Simon Msuva na Thabani Kamusoko wakifunga kwa upande wa Yanga.

Kwa maana hiyo Simba ambayo ni mabingwa mara tatu wa michuano hiyo itacheza fainali na Azam FC siku ya Ijumaa huku wenyewe wakitinga fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Taifa Jang'ombe kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyopigwa jioni.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kiasi ambapo timu zote zilishambuliana kwa zamu huku zikicheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha nyavu zao hazitikiswi na mpira ukichezwa zaidi eneo la katikati ya uwanja.

Kiungo Mohammed Ibrahim wa Simba alipata nafasi ya kufunga dakika ya 43 na shuti lake la mguu wa kushoto likagonga mwamba huku Juma Liuzio akishindwa kumalizia baada ya mpira kumfuata mguuni.

Kocha wa Simba Joseph Omog ambaye muda mwingi wa mchezo alikuwa amesimama kutoa maelekezo kwa wachezaji wake aliwatoa Shiza Kichuya,Liuzio na Ibrahim nafasi zao zikachuliwa na Jamal Mnyate, Pastory Athanas pamoja Laudit Mavugo huku Yanga ikimuingiza Emmanuel Martin kuchukua nafasi ya Deus Kaseke.

Huu unakuwa mchezo wa tano baina ya timu hizo kukutana kwenye uwanja huo ambapo Simba wameshinda mechi nne na Yanga wakiibuka na ushindi mara moja.

Post a Comment

kim da yu mbwana said... 10 January 2017 at 23:37

Pongezi kwa wachezaji benchi la ufundi viongozi wanachama na mashabiki wa Simba sc mapambano yanaendelea azam your next.


 
Top