BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

YANGA wametolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa na Simba kwa mikwaju ya penalti 4-2 lakini wao wamesema kuwa michuano hiyo wameitumia kama mazoezi ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na michuano ya kimataifa.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa VPL wanajiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika na sasa tayari wamerejea jijini Dar es Salaam baada ya kufungashiwa virago katika hatua ya nusu fainali ambazo zimechezwa jana Jumanne kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Pamoja na kwamba Yanga nao walionekana kuwa na hamu ya kutinga fainali lakini hesabu zao zilishindwa kukaa sawa baada ya watani zao kuwazidi ujanja kwenye penalti huku dakika 90 zikiwa zimemalizika kwa sare tasa.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' amesema kuwa jambo kubwa walilonufaika nalo ni kujipa mazoezi ya kutosha kupitia mashindano hayo na kuwapongeza watani wao kufika hatua hiyo.

"Hakuna mchezo usiokuwa na makosa, hivyo ndivyo mpira ulivyo, mashindano yalikuwa mazuri na tunawatakia kheri waliofika hatua hiyo na wafanikiwe kutwaa ubingwa.

"Tumetumia mashindano hayo kama njia ya kufanya mazoezi kwa ajili ya michuano ya kimataifa iliyopo mbele yetu pamoja na mechi za ligi kuu, hivyo tumepata faida kwa hilo na hakuna mchezo usio na makosa," alisema Canavaro.

Simba na Azam zitakucheza fainali hizo za maadhimisho ya siku ya Mapinduzi ya Zanzibar keshokutwa Ijumaa. Azam wao wameingia baada ya kuifunga Taifa Jang'ombe bao 1-0.

Post a Comment

Mick Dadd Simbeye said... 12 January 2017 at 01:10

ongereni sana simba lakini mjiandae kwa azam

 
Top