BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu, Zanzibar

KIUNGO Frank Domayo ameonyesha kwanini aliitwa 'Chumvi' kutokana uwezo mkubwa wa kunogesha mechi baada ya kuiwezesha timu yake ya Azam FC kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi akifunga bao pekee dhidi ya Taifa Jang'ombe huku kocha mpya wa timu hiyo, Aristica Cioaba raia wa Romania akitamka kukisuka kikosi hicho na kuwa tishio barani Afrika.

Domayo alifunga bao hilo dakika ya 33 kwa shuti kali alilopiga kwa mguu wa kushoto akiwa nje ya eneo la 18 ambapo mabeki wa Jang'ombe walishindwa kuokoa hatari hiyo ikiwa ni mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar huku Domayo akitangazwa Mchezaji Bora wa mechi hiyo.

Taifa Jang'ombe walirudi kwa kasi ya kutaka kusawazisha bao hilo kipindi cha pili lakini safu ya ulinzi ya Azam iliyokuwa chini ya Yakub Mohammed na Agrey Moris ilikuwa makini kuhakikisha mlinda mlango wao Aishi Manula anakuwa salama muda wote.

Mwamuzi Mohamed Kassimu alimuonyesha kadi ya njano beki wa Azam, Gadiel Michael ikiwa ni kumuonya baada ya kumchezea rafu kiungo Arafat Abdallah dakika ya 64 ambapo wengi waliamini angetolewa nje kwa kadi nyekundu huku Gadiel akishindwa kufunga bao la pili dakika ya 84 baada ya shuti lake kugonga mwamba.

Azam itacheza mchezo wa fainali Ijumaa, Januari 13 na mshindi kati ya timu za Simba na Yanga zitakazokutana muda mfupi ujao katika mchezo wa nusu fainali ya pili utakaochezwa kwenye uwanja huo.


Wakati huo huo, kocha Cioaba ayekabidhiwa mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, kwa mkataba wa miezi sita ameshuhudia mechi hiyo alisema kuwa anafuraha kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo huku akiahidi kazi nzuri na kuifanya kuwa bora katika michezo ya kitaifa na kimataifa.

“Najua Azam ni miongoni mwa klabu kubwa hapa Tanzania napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri.

“Kuhusu wakati ujao, nina furaha sana uongozi walipozungumza na mimi wakati tunaweka mipango ya timu ya hapo baadaye na hili ni jambo zuri kwa kocha, kitaaluma nawaahidi mashabiki na watu wote wanaoipenda Azam niko hapa kuwapa mambo mazuri katika kazi yangu kwenye klabu,” alisema Cioaba.

Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Ghana ambapo anafahamiana kwa ukaribu na nyota wawili wa Azam, Yakubu Mohammed na Yahaya Mohammed, waliosajiliwa kutoka timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo.

Mbali na kufundisha soka nchini Ghana pia amewahi kufanya kazi kwenye miamba ya Morocco, Raja Casablanca, Al Masry ya Misri na katika nchi za Romania, Kuwait, Oman na Jordan.

Mromania huyo ataiongoza Azam kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa msimu ambapo watakaa tena mezani kufanya tathimini ya mafanikio yake ili kuona kama wataweza kuendelea nae.

Post a Comment

 
Top