BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi,Dar
TIMU ya Friends Rangers imefufua matumaini ya kupanda ligi kuu Tanzania bara baada ya kuifunga Ashanti United mabao 2-1 kwenye mchezo wa kundi A ligi daraja la kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Karume Dar es Salaam.

Rangers imefikisha pointi 16 alama saba nyuma ya vinara Lipuli huku wakisalia na michezo minne kabla ya kuhitimisha ligi hiyo yenye ushindani mkubwa kwakua timu zote zimekuwa zikipigana vikumbo ili kupanda ligi kuu.

Ashanti  walikua wakwanza kupata bao lililofungwa na Hussein Mkongo dakika ya 27 ambalo lilidumu hadi  mapumziko. 


Kipindi cha pili  Rangers waliingia kwa kasi kubwa mithili ya mbogo aliyejeruhiwa kwa kukafanya mashambulizi mfululizo  langoni mwa Ashanti lakini washambuliaji wake walikosa utulivu.

Dakika ya 77 mchezaji Ngate Chanai aliisawazishia Rangers  kwa kichwa baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Musa John bao lililorejesha morali ya mchezo kwa timu zote.

Chanai tena alifunga bao la ushindi dakika ya 82 baada ya mlinda mlango wa Ashanti Rajabu Kaumbu kutema shuti kali lililopigwa na kiungo Haruna Moshi 'Boban' kabla ya mfungaji huyo kuutumbukiza wavuni.

Post a Comment

 
Top