BOIPLUS SPORTS BLOG


Karim Boimanda
www.boiplus.blogspot.com
DAWA nyingi zina ladha chungu lakini kama unataka kupona basi piga moyo konde uzimeze tu, hakuna namna. Hii haina tofauti na mtu muoga wa kupanda ndege na asiyetaka kusikia kuhusu kusafiri kwa boti anatamani kuingia uwanja wa Amaan leo kushuhudia mechi kati ya Yanga na Azam.

Ukiwa kwenye Uwanja wa Taifa wakati timu moja kati ya Yanga na Simba inacheza unaweza kustaajabu ni kanuni gani imetumika kuwapanga mashabiki wa timu hizi, si rahisi kuona rangi nyekundu katika jukwaa la Yanga na ukiona jezi ya kijani kwenye jukwaa la Simba basi rudi kitandani ukalale kwa maana utakuwa unaota.

Azam nao licha ya kuwa na mashabiki wachache wameshaingia kwenye 'siasa' hizi ambazo nchi kama Afrika Kusini na nyingi barani Ulaya hakuna kabisa, mashabiki wa timu pinzani hujichanganya na kufurahia mchezo kama 'kawa'.

Leo nimeamka kibabe na nataka hizi timu tatu zianze japo kuigana hasa kwenye yale mazuri, nataka Azam watoke Chamazi wawapitie Simba pale Msimbazi halafu waongozane kwenda mitaa ya Twiga na Jangwani pale Kariakoo kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja na Yanga.

Umetimia mwaka mmoja na siku mbili tangu Yanga wavaane na Azam katika mchezo wa kundi B wa kombe la Mapinduzi kwenye dimba la Amaan visiwani Zanzibar. Nakumbuka Kipre Tchetche aliipatia Azam bao la kwanza dakika ya 58 kabla Vincent Bossou hajasawazisha dakika ya 82 na kufanya mchezo huo uishe kwa sare ya bao moja.Kumbukumbu zangu zilienda mbali zaidi hadi kwenye vikosi vilivyopambana siku hiyo, na hapo ndipo 'gubu' la Mzee wa Black & White lilipolipuka. Kikosi cha Yanga ambacho kilianza siku hiyo kinamkosa mchezaji mmoja tu leo ambaye ni Mbuyu Twite, wakati Azam wao kitawakosa nyota watano kwa maana wamebakia sita tu katika waliocheza siku hiyo.

Katika kikosi hicho Azam kulikuwa na msenegali Raccine Diouf, waivory Coast Pascal Wawa na Kipre Tchetche, Mnyarwanda Jean Babtiste Mugiraneza 'Migi' na Ame Ally ambao walibeba mabegi yao huku wakibaki Aishi Manula, Shomari Kapombe, Abdallah Kheri, Himid Mao, John Bocco na Ramadhan Singano pekee.

Wachezaji hao watano wanaokosekana ni tofauti na ambao walikuwa benchi siku hiyo pamoja na ambao walisajiliwa baada ya kombe la Mapinduzi mwaka jana na kutemwa kabla ya Mapinduzi mwaka huu, Azam nyie sio watu wa mchezo mchezo, hebu wapitieni ndugu zenu Msimbazi pale mkaombe ushauri Jangwani, hakuna namna.

Kitaalamu kitendo hiki cha kubadili kikosi mara kwa mara hakileti afya nzuri ya timu badala yake kinazidi kudhoofisha. Ukiwatazama Yanga wanavyocheza utagundua wamezoeana na hii huwasaidia kuficha hata udhaifu wao pale wanapozidiwa. Naamini katika kikosi chao cha leo kitakuwa na wachezaji wapya wasiozidi watatu tu ukilinganisha na kile kilichoshuka dimbani mwaka jana dhidi ya Azam uwanja wa Amaan. Wafuateni wawapeni siri, ujinga wakati wa kwenda tu...Januari 10 mwaka jana katika michuano hiyo hiyo Simba iliondolewa kwenye hatua ya nusu fainali baada ya kupigwa bao 1-0 na Mtibwa, sina nia ya kuwakumbusha machungu bali nimekumbuka tu kikosi cha siku ile nikakifananisha na ambacho kimekuwa kikitumika kwenye michuano ya mwaka huu.

Wachezaji tisa kati ya 18 walioshiriki katika mchezo huo tayari hawapo kwenye kikosi hicho ambao ni Emery Nimubona, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Awadh Juma, Mussa Mgosi (Meneja), Danny Lyanga, Khomeiny Baruan, Paul Kiongera na Hamis Kiiza. Aisee Azam wakija hapo msikatae kwenda nao Jangwani kuomba dawa ya huu ugonjwa tafadhali.

Sidhani kama kuna sayansi ya kutisha Yanga wanaitumia zaidi ya kuheshimu taaluma za makocha na kufuata taratibu za usajili pamoja na kuwa na moyo wa subira. Hata kama Yanga pia wana gonjwa la viongozi kusajili badala ya makocha hawana hali mbaya kama Simba na Azam, Yanga bado wana nafuu katika kufuatilia wachezaji kabla ya kuwasajili pamoja na tabia njema ya kuvumilia wachezaji.

Kama si subra ya Yanga, Bossou na Obrey Chirwa wasingekuwemo kikosini lakini pia utaona mchezaji kama Paul Nonga, licha ya kukosa nafasi bado Yanga hawakuonyesha nia ya kumuacha hadi pale yeye mwenyewe alipoomba kuondoka. Azam, Simba fanyeni tafakari ya haya kisha fanyeni maamuzi hata kimya kimya, kwenye hili Yanga wameweza, waigeni tu sio 'issue'.


Maoni;
Mob: +255788334467
E-mail: karim@boiplusmedia.com

Post a Comment

 
Top