BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Zanzibar

"Lwandamina utaua...." ni kauli ya shabiki mmoja aliyoitoa baada ya kuona kocha George Lwandamina anawainua viberenge Juma Mahadhi na Deus Kaseke waingie kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi kati ya Yanga na Jamhuri ambao Yanga waliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 katika dimba la Amaan Zanzibar.

Wakati mawinga hao wanainuliwa tayari Jamhuri walikuwa wameshapoteana kwa mvua ya mabao iliyoanza dakika ya 19 baada ya Simon Msuva kumalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima kabla Donald Ngoma hajapachika la pili dakika nne baadae kwa krosi ya Haji Mwinyi.

Ngoma na Msuva waliendelea kuiadhibu Jamhuri kwa mabao ya dakika za 37 na 40 huku wenyeji hao wa kisiwa cha Pemba wakimaliza dakika 45 za mwanzo bila kupiga hata shuti moja langoni mwa Yanga.

Kipindi cha pili Yanga waliendelea kucheza kwa nguvu wakionyesha uchu zaidi wa kuzifumania nyavu za wapinzani wao na dakika 59 Kamusoko alipiga msumari wa tano kabla Mahadhi hajafunga kitabu cha mabao dakika ya 85.

Licha ya safu ya kiungo ya Yanga kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa, kiungo wa Jamhuri Greyson Gerald alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi kutokana na jinsi alivyojitahidi kuwapunguza kasi watoto hao wa Jangwani.

Post a Comment

 
Top