BOIPLUS SPORTS BLOG


Mwandishi Wetu, Zanzibar
STRAIKA wa Simba Laudit Mavugo leo amemaliza ukame wa mabao kwa staili ambayo ni kama kuichonganisha timu yake na Yanga baada ya kupachika mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Jang'ombe Boys uliowaweka wekundu hao kileleni mwa kundi A.

Yanga walitangulia nusu fainali kutokea kundi B licha ya kichapo cha mabao 4-0 walichokipata jana dhidi ya Azam na kushika nafasi ya pili hivyo kwa mujibu wa ratiba wapinzani hao wa jadi watakutana jumanne usiku katika mchezo wa nusu fainali.

Mavugo aliyetangazwa mchezaji bora wa mechi hiyo aliipatia Simba bao la kwanza Simba kwenye uwanja wa Amaan akimalizia kiulaini mpira uliopanguliwa na kipa wa Jang'ombe kufuatia shuti la Shiza Kichuya dakika ya 11 kabla hajapachika la pili kwa shuti kali dakika 54 baada ya kujitangulizia mpira kwa kisigino.

Kocha Joseph Omog aliwatoa nyota wake Mavugo, Juma Liuzio, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya na Janvier Bokungu huku nafasi zao zikichukuliwa na Jamal Mnyate, Hija Ugando, Moses Kitandu, James Kotei na Vicent Costa ikiwa ni dalili ya kuwapumzisha kwa ajili ya mchezo mgumu dhidi ya Yanga.

Mchezo wa mwisho wa kundi B utapigwa saa 2:30 usiku huu kati ya Taifa Jang'ombe na URA ambapo kama URA watashinda basi watatinga nusu fainali moja kwa moja lakini Taifa Jang'ombe wakishinda itaangaliwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baina yao na Jang'ombe Boys ambao nao pia wana pointi sita.

Post a Comment

 
Top