BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Zanzibar

WINGA wa Yanga Simon Msuva leo amepachika mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 walioupata dhidi ya Zimamoto kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi uwanja wa Amaan.

Mabao hayo yamemfanya winga teleza huyo afikishe jumla ya mabao manne na kuongoza katika orodha ya wafungaji bora baada ya kuwa alifunga mengine mawili kwenye mchezo wa kwa dhidi ya Jamhuri.

Msuva alipachika bao la kwanza dakika ya 11 akimaliza mpira wa adhabu ndogo uliopigwa kiufundi na Haruna Niyonzima ambaye kiwango chake katika siku za hivi karibu kimewapagawisha wadau wengi wa soka.

Dakika ya 21 kiungo Thaban Kamusoko alipiga mpira mrefu kutokea eneo la kati ya uwanja ambao ulinaswa na mchezaji bora wa mechi hiyo, Msuva ambaye alimchambua kipa wa Zimamoto na kupachika bao la pili.

Ikionekana kama mechi hiyo ingemalizika kwa Yanga kutoa dozi nzito, vijana wa Zimamoto walitulia hasa kipindi cha pili na kufanikiwa kuvuruga mipango mingi ya Yanga ingawa wenyewe hawakuonekana wenye madhara langoni mwa vijana hao wa Jangwani.

Golikipa wa Zimamoto Mwinyi Hassan Hamisi aliokoa penalti iliyopigwa na Msuva dakika ya 50 baada ya winga huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari.


Yanga wanaongoza kundi B wakiwa na pointi sita wakifuatiwa na Azam FC wenye alama tatu ambao watashuka dimbani saa 2 usiku kucheza na timu ya Jamhuri.

Post a Comment

 
Top