BOIPLUS SPORTS BLOG


Mwandishi Wetu, Zanzibar
BEKI mkongwe wa Simba raia wa Zimbabwe, Method Mwanjali leo amethibitisha tena kuwa anastahili kuitwa 'Baba mwenye nyumba' baada kuonyesha umahiri mkubwa kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi dhidi ya URA uliomalizika kwa sare tasa.

Mlinzi huyo mtulivu alifanikiwa kuzima hatari zote zilizoelekezwa langoni mwao hali iliyolishawishi jopo la makocha kumtangaza mchezaji bora wa mechi ikiwa ni mara ya pili katika michuano hiyo inayoendelea kwenye dimba la Amaan hapa visiwani Zanzibar.

Washambuliaji wa URA ambao walionekana kutumia nguvu nyingi walishindwa kuziona nyavu za wekundu hao sawa na nyota wa Simba walivyoishia kulitazama tu lango la URA huku mpira wa kasi na nguvu ukichezwa katika dakika zote 90 za mchezo.

Kwa kuchaguliwa mchezaji bora wa mechi Mwanjali amezawadiwa katoni nne za kinywaji cha Azam Malt kinachotengenezwa na kampuni ya Bakhressa Food Products huku nahodha Jonas Mkude akipokea zawadi hiyo kwa niaba yake.

Simba itamaliza mchezo wa mwisho hatua ya makundi kwa kumenyana na Jang'ombe Boys huku URA ikimaliza na Taifa Jang'ombe.

Post a Comment

 
Top