BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Zanzibar

MARA ya mwisho kufundisha soka nchini kocha Joseph Omog aliiwezesha Azam FC kubeba kombe la ligi kuu ya Vodacom lakini Mcameroon huyo ameonyesha licha kulenga kombe hilo akiwa na Simba, anataka kuwapa kwanza kombe la Mapinduzi baada ya leo kuanza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Taifa Jang'ombe.

Mchezo huo wa kwanza kwa Simba kwenye michuano hiyo na wa pili kwa Jang'ombe ulichezwa kwenye uwanja wa Amaan mjini Zanzibar huku timu hizo zikionyesha kandanda linaloshabihiana ambalo ni la pasi za chini na kasi.

Simba ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lililowekwa nyavuni dakika ya 27 na kiungo anayetisha kwa mabao, Mzamiru Yassin akimalizia mpira uliogonga mwamba na kurejea uwanjani kufuatia shuti kali la Method Mwanjali.

Juma Liuzio

Jang'ombe licha ya kuonyesha soka safi walijikuta wakipachikwa bao la pili na mshambuliaji Juma Liuzio aliyewazidi nguvu na kasi mabeki wao dakika ya 41 na kufanya Simba waende mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Jang'ombe kufanya mashambulizi kadhaa huku wakiiweka kwenye wakati mgumu ngome ya Simba ambapo katika dakika ya 76 beki Novaty Lufunga alijifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa kona.

Kwa ushindi huo Simba wanashika nafasi ya pili katika kundi lao linaloongozwa na URA kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufunga huku Jangombe wakiwa katika nafasi ya tatu kila moja ikiwa na pointi tatu. Jang'ombe Boys na KVZ zinaburuza mkia baada ya kupoteza mechi zao za mwanzo.

Post a Comment

 
Top